Vitunguu ni zao la mbogamboga na hulimwa kwa ajili ya balbu zake. Hulimwa nyanda za baridi kwa wingi sana. Nyanda zenye joto vitunguu hulimwa pia. Tanzania vitunguu hulimwa sana sehemu za Mang'ula, Mgeta na Singida. Hata hivyo vitunguu hustawi maeneo mengi ya Tanzania.Vitunguu vinaweza kulimwa mwaka mzima endapo maji yanapatikana.Vitunguu vina matumizi mengi sana na vina madini joto, chuma, vitamin A, vitamin B, vitamin C na vitamin E


  MAELEZO YA MSINGI KUHUSU KILIMO CHA VITUNGUU.
1.Hali ya joto.
Joto  linatakiwa  sana  kwa  ajili  ya  ukuaji  wa  balbu  ila  joto  likizidi  vitunguu  hukomaa  mapema  kabla  balbu hazijafikia ukubwa unaostahili, hivyo mkulima anaweza kupata mazao kidogo. 
2.Udongo na mahitaji ya maji
Vitunguu huweza kupandwa kwenye udongo wowote wenye rutuba, usiotuamisha maji na usionata sana.
Hufanya vizuri kwenye udongo wenye aside kidogo japo udongo wenye alkali kidogo sio mbaya sana. Kwenye udongo wenye mchanga mchanga umwagiliaji ni lazima.
Udongo mzuri sana kwa ustawi wa vitunguu ni tifutifu kichanga.Umwagiliaji ni muhimu sana hasa wakati wa kuanza kutengeneza balbu. Unyevu uliozidi ni hatari sana kipindi cha ukuaji.
Epuka matumizi ya mbolea mbichi isioiva vizuri kwani husababisha vitunguu kuwa na shingo pana sana majani hukua sana badala ya balbu.
3.UZALISHAJI NA UPANDAJI WA VITUNGUU
Kabla ya kupanda udongo ni lazima utifuliwe vizuri na reki kuondoa mabaki ya mimea na mawe ama Vipande vikubwa vya udongo. Matuta yawe na upana wa mita moja. Vitunguu hupandwa kwa mstari mojakwamoja ama kutokea  kitaluni.  Pia  huweza  kupandwa  kwa  mstari  pacha.    Vitunguu  hupandwa  sm10-15  kutoka  mmea  hadi mmea na  sm 10-15 kutoka mstari hadi mstari, kama inavyoonekana kwenye mchoro hapa chini.
Mfano wa tuta la vitunguu
EPUKA
Kununua  mbegu  za  mitaani,  kuzidisha  sana  mbolea  na  umwagiliaji  usio  na  mpangilio  kwani  husababisha vinguu kuzaa pacha.
Pia  epuka  kupanda  vitunguu  mahali  palipopandwa  mboga  jamii  ya  vitunguu  siku  za  nyuma.  Mfano  Vitunguu saumu na vitunguu majani.
KITALU CHA VITUNGUU
Ni muhimu kumwagilia maji ya kutosha siku kumi za mwanzo tangu kusia mbegu kitaluni. Vitunguu hukaa kitaluni kwa wiki 6-8 na miche ifikiapo upana wa penseli na urefu wa sm 15 ni tayari kwa kuhamishia shambani/bustanini


AINA ZA VITUNGUU VINAVYOLIMWA TANZANIA
  • Red Creole
  • Bombay Red
  • Hybrid F1 
MAHITAJI YA MBOLEA
Vitunguu  hufanya  vizuri  kama  shamba  litawekewa  mbolea  ya  samadi  ama  mboji  ilioiva  vizuri. Kiasi  cha  tani 25-40 kwa heka kinashauriwa. Hii ni sawa na kilo 7.5-12 kwa tuta lenye urefu wa mita 3 na upana wa mita 1.
UVUNAJI

Vitunguu  huvunwa  kuanzia  siku  90-150  tangu  kusia  mbegu.  Dalili  za  kukomaa  ni  kuanguka  kwa  majani.
Vitunguu  huvunwa  kwa  kuvuta  kwa  mkono  na  kuhifadhiwa  siku  kadhaa  shambani  vikiwa vimefunikwa  na majani. Baada ya hapo majani hukatwa na balbu hupakiwa kwa ajili ya kuhifadhi kusubiria bei nzuri. Vitunguu huweza kuhifadhiwa hadi miezi 9 tangu vivunwe bila kuharibika. Vitunguu vihifadhiwe kwenye nyuzijoto chini ya 4.4 °C ama juu ya nyuzijoto 25°C ili visiharibike.
UTUNZAJI WA SHAMBA
Kutandazia  shamba  na  majani  yaliyooza  vizuri  ama  mabua  inashauriwa  ili  kuongeza  ruba  ya  ardhi,  zuia magonjwa  yatokanayo na udongo na magugu. Kupanda vitunguu kwenye matuta  yaliyoinuka ni  muhimu sana kuzuiya  utuamishaji  wa  maji  na  mlipuko  wa  magojwa  ya  miche.  Kungoa  magugu  na  uvunaji  ufanywe  kwa mkono.
 

 


UUZAJI
Vitunguu   ni   zao   lenye   bei   nzuri   ukilinganisha   na   mazao   mengine   ya mbogamboga  na  huuzwa  kwenye  masoko  ya  kawaida  kwa  bei  nzuri.  Kwa  hivi sasa hapa  Morogoro  vitunguu  kilo  moja  ni  Tshs1500/=.  Kama vitunguu vikilimwa vizuri na kuhudumiwa ipasavyo Ekari moja huzaa gunia 70-90  sawa  na  kg 7000-9000.  Kama  akipata  soko  la  uhakika  mkulima  anaweza kupata hadi 13.5 milioni kwa msimu mmoja.
MAKALA HII IMETAYARISHWA NA:-
BUSTANI YA TUSHIKAMANE KILIMO HAI
Tushikamane Centre, Kilakala Road
Morogoro Tel: +255765 596255